Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima akitoa hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kwenye Hoteli ya Intercontinental jijini Muscat hivi karibuni. Pamoja Mhe. Balozi Kilima aliuelezea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuwa ni kielelezo muhimu kinachoonesha kwa vitendo nia thabiti ya Serikali ya Tanzania kuimarisha umoja na mshikamano miungoni mwa nchi za Afrika na kwamba ndio iliyokuwa azma ya waasisi wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati, Rais Abeid Amani Karume.
Mhe. Balozi Kilima alieleza kuwa katika miaka 55 ya Muungano, Tanzania imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta za uchumi, elimu, biashara, uwekezaji na huduma za jamii kama vile afya na upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Alieleza pia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inaendeleza jitihada za kujenga mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji, jitihasa hizi zinahusisha kujenga misingi ya utawala bora, kupambana na rushwa na ufisadi na kujenga utumishi wa umma wenye maadili na viwango. Balozi Kilima alitumia nafasi hiyo kuwaomba wafanyabiashara wenye nia kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji kwa kuwekeza na kuanza biashara Tanzania. Wakati wa hafla hiyo Ubalozi uligawa vipeperushi mbalimbali kwa wageni waalikwa kuhusu utalii, uwekezaji pamoja na taarifa mbalimbali kuhusu Tanzania.